SHUGHULI za kisiasa kule Mombasa zimesimama kwa muda na shauku kubwa ya wananchi ni kumuona mkali wa Bongo Flava, Aki Kiba akimfunua shela mrembo, Amina Khaleef kisha kumvisha pete ya ndoa kidoleni na kumwambia wewe ndio mke wangu wa maisha.
Amsha amsha za ndoa hiyo itakayofungwa kesho Alhamisi kwenye ukumbi wa maraha wa Diamond Jubilee mjini Mombasa, zinazidi kupamba moto.
Habari za kuaminika zinasema kwamba, tayari Kiba na familia yake ikiwemo mshkaji wake wa karibu, Ommy Dimpoz pamoja na timu nzima ya Rockstar imetua hapa nchini jana usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Mrembo Amina ambaye anatokea Mtaa wa Kongowea, familia yake ina uhusiano wa karibu na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho.
Gavana huyo ambaye awali alikuwa Mbunge wa Kisauni, ambako Amina alikuwa akiishi pia, ni rafiki wa karibu na Kiba. Inaaminika kuwa Joho ndio amesaidia kwa kiasi kikubwa kumuunganisha Kiba na familia ya Amina, ambapo safari zake za mara kwa mara mjini Mombasa, hazikuwa kwa shughuli za kimuziki tu bali ni kuwa karibu na mkewe huyo mtarajiwa.
Harusi hiyo inatarajiwa kurushwa laivu kwenye luninga na Azam kuanzia Mombasa ambako Joho na vigogo wengine wa Muungano wa NASA wanatarajiwa kuhudhuria huku sherehe ya hapa nchini, Tanzania itahudhuriwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na viongozi wengine.
No comments:
Post a Comment