Mabosi kuwapa Sh 100 mil wachezaji Yanga
MABOSI wa Yanga wamekaa na wachezaji wao katika kikao kifupi usiku wa jana Jumanne na walipomaliza kila mchezaji alitoka anacheka huku wakihamasishana kufanya kweli katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Wolaitta Dicha ya Ethiopia.
Na baada ya kufanya uchunguzi ili kujua kilichowaongezea morali, kumbe jamaa wameahidiwa mshiko wa maana endapo tu watashinda ambapo ni kiasi cha Sh 100 mil 'keshi'.
Tena aliyevujisha 'inshu' hiyo ni nahodha wao, Nadir Haroub 'Cannavaro' na akasisitiza wao walishajipanga lakini kutokana na ahadi hiyo wanataka kumaliza kazi mapema.
"Ni kweli tulikutana na viongozi, kilikuwa kikao kizuri na kila mmoja wetu amefurahi, tumezungumza mengi na hiyo ahadi unayosema ilitolewa ingawa yapo mengi zaidi tumeambiwa na uongozi,"anasema Cannavaro ambaye ni beki wa kati.
Waliotoa ahadi hiyo ni mabosi wao waliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Hussein Nyika na wajumbe wake Samuel Lukumay na Hamad Islam ambao wako na timu hapa Hawassa.
Mabosi hao waliwaambia wachezaji wao wapambane kuhakikisha timu inaingia hatua ya makundi pia mbali na ahadi hiyo, watarekebishiwa mambo yao mengi ya kimaslahi mara tu watakapowasili nchini.
Yanga inacheza na Wolaitta leo Jumatano nchini Ethiopia ikiwa ni marudiano baada ya mchezo wa kwanza vijana wa Jangwani wakimaliza na ushindi wa mabao 2-0. Yanga inahitaji sare ya aina yoyote waendelee kusonga hatua ya makundi ya mashindano hayo.

No comments:
Post a Comment